Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amesema, hakuna tofauti kati ya kile Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu anakifanya katika mashambulizi ya miezi kadhaa sasa huko Gaza na kile kiongozi wa Nazi Adolf Hitler alichokifanya miongo kadhaa iliyopita.

Akihutubia katika hafla ya utoaji tuzo ya Sayansi iliyofanyika mjini Ankara, Erdogan alimtuhumu  Netanyahu kwa kumuuliza: “hivi wewe (Netanyahu) unatofautianaje na Hitler? Watatufanya tufikirie kuwa uovu wa Hitler ni mdogo zaidi. Lakini je, kuna chochote anachofanya Netanyahu ambacho ni kidogo kuliko Hitler? Hapana.”

Aidha, amelinganisha jinsi wanavyotendewa duniani kote wasomi wanaothubutu kukemea ukandamizaji na mateso yanayofanywa leo na yaliyofanywa Ujerumani ya Nazi miaka 80 iliyopita.

“Kugeuzwa mbuzi wa kafara” kumeanzishwa dhidi ya mtu yeyote anayeikosoa Israel, ikiwa ni pamoja na wanachuo katika taasisi nyingi za kimataifa za elimu”, amesema Erdogan.

Erdogan amebainisha kuwa, wasomi nchini Marekani na kwingineko wanafukuzwa kazi au kulaumiwa kwa kuwatetea Wapalestina, na pia kukabiliwa na mashinikizo na vitisho, sawa na wale waliowatetea Wayahudi miongo kadhaa iliyopita.

Katika hotuba yake hiyo, rais hyyo wa Uturuki ameeleza kuwa, kuanzia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hadi mashirika ya habari, Umoja wa Ulaya mpaka makundi ya waandishi wa habari pamoja na asasi zote zinazotumika kama vinara wa demokrasia, zimefeli katika kukabiliana na mashambulio ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza.

“Hivi unaweza kufikiria marais wa vyuo vikuu wanahojiwa na kuwajibishwa katika Kongresi kwa sababu tu wanatetea haki za watoto, wanawake na raia?” amehoji Erdogan, akimaanisha marais wa vyuo vikuu vya Harvard, Pennsylvania na MIT, ambao mnamo Desemba 5 walifikishwa mbele ya bunge la Marekani ili kusailiwa kuhusiana na tuhuma za kuwepo uenezaji chuki dhidi ya Uyahudi kwenye vyuo vikuu hivyo.

Aidha amesema kuwa ukosoaji mdogo kabisa unaofanywa hata ndani ya mipaka ya sheria na demokrasia unakandamizwa kwa kibandikwa chapa ya chuki dhidi ya Wayahudi, na unachukuliwa kuwa ni kosa la jinai.

Aidha amekiri kuwa, licha ya juhudi za kidiplomasia zilizofanywa na nchi zenye dhamiri kama Uturuki, kwa bahati mbaya, imeshindikana hadi sasa kuzuia mauaji ya mamia ya watu wanaouawa kila siku huko Ukanda wa Gaza.

Duru rasmi za Palestina zimetangaza kuwa, hadi sasa Wapalestina zaidi ya 21,000 wameuawa shahidi kutokana na mashambulio ya kinyama yanayoendelea kufanywa na jeshi la kigaidi la utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel.

Idadi ya waliofariki kwa mlipuko wa Lori yaongezeka
Benchikha abadili mpango usajili Simba SC