Ama kweli vituko Duniani haviwezi kuisha, kwani kwa wale ambao wamebahatika kufika jijini Tokyo Nchini Japan au wale ambao ni wadadisi wa mambo, bila shaka walipata simulizi au kusoma habari za Mgahawa mmoja ambao wengi wa wahudumu wake hawana kumbukumbu.

Inaarifiwa kuwa mteja akifika Mgahawani hapo, huletewa chakula tofauti na kile alichoagiza na suala hilo ni kawaida sana kiasi ikapelekea jina la Mgahawa huo kuitwa “Restaurant For Mistake Orders.”

Ipo hivi, mteja anaweza agiza Vibanzi na Kuku halafu akaletewa Sharubati ya Tufaa, au akaagiza Supu ya Kongoro, halafu akaletewa Maandazi kitu ambacho kitampa mshangao na kibaya zaidi Wahudumu wengi wa Mgahawa huo umri umewatupa mkono.

Mbele ya lango la Mgahawa huo, kuna bango linalosomeka, “Wahudumu wa Mgahawa huu hawana kumbukumbu, hivyo utakula na kulipa kilicho letwa.” wakimaanisha utakula kile alicholeta Muhudumu na si ulichoagiza wewe kama mteja.

Inasimuliwa kuwa asilimia 90 ya oda ya vyakula inayotolewa na wateja ni tofauti na ile inayopelekea mezani na cha kustaajabisha licha ya kuwa oda zinazo tolewa ni tofauti na zinazo agizwa na wateja bado wao hufurahia na kuona ni kichekesho kisha kuendelea na mlo kama kawaida.

Inasemekana wateja hufurahia na hupenda sana kwenda kwenye Mgahawa huo, kwani huona hiyo ni kama sehemu ya kichekesho na hivyo kufurahia wanapopita au wanapoingia kupata huduma ili kuona nini kitaletwa baada ya kutoa oda.

Kuna wakati Mmiliki wa Mgahawa huo, aliwahi ulizwa ni kwanini amewaajiri watu wenye kupoteza kumbukumbu, akajibu kuwa amefanya hivyo kama sehemu ya kuwachangamsha akili watu wenye shida hiyo na ikiwa ni sehemu pia ya kuwaondolea mawazo.

Twaha Kiduku: Nitajirekebisha 2024
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Desemba 28, 2023