Idadi ya watu waliopoteza maisha katika mlipuko wa Lori la mafuta uliotokea katikati ya Nchi ya Liberia imeongezeka na kufikia watu 40.

Francis Kateh, Afisa Mkuu wa Afya wa nchi hiyo, alisema makumi ya watu wengine wamejeruhiwa kwenye mkasa huo uliotokea baada ya lori la mafuta kupinduka na kuanguka kwenye mtaro kando ya barabara mjini Totota, Kaunti ya Bong.

Amesema idadi ya wahanga wa ajali hiyo ya Jumanne ikaongezeka kutokana na hali mbaya ya mejeruhiwa waliolazwa hospitalini.

Aidha Afisa wa Afya wa Kaunti ya Bong, Dkt. Cynthia Blapooh ameliambia gazeti linalochapishwa nchini humo la Front Page Africa kwamba, “bado tuna wagonjwa wengi waliojeruhiwa vibaya wakiwemo watoto na mwanamke mjamzito. Tumepokea jumla ya majeruhi 36.”

Kwa upande wake, Malvin Sackor, Afisa wa Polisi katika eneo hilo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, “Lori la mafuta lililokuwa limesheheni petroli lilipinduka na watu katika eneo hilo wakaanza kuchota mafuta, hali iliyopelekea lori hilo kuripuka na kuua na kujeruhi watu wengi.”

Naye Aaron Massaquoi, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, lori hilo la mafuta liliposhika moto baada ya kuripuka, watu waliokuwa juu yake wakijaribu kuchota mafuta waliungua kiasi cha kutotambulika.

Miundombinu mibovu na upuuzaji wa sheria za usalama barabarani vimeifanya Liberia kuwa moja ya nchi za chini ya eneo la jangwa la Sahara barani Afrika zinazapoteza maelfu ya watu katika ajali za barabarani kila mwaka.

JKT Tanzania yavuta kifaa kutoka Zenji
Hakuna tofauti kati ya Hitler na Netanyahu: Rais Erdogan