Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula ameonesha kutoridhishwa na kasi ya wananchi wanaojitokeza kuchangamkia kuchukua hati za ardhi kwenye zoezi la urasimishaji katika halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Ameyasema hayo wakati akitoa hati 101 kwa wananchi wa wilaya ya Bukoba wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi mkoani Kagera.

Amesema pamoja na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt, John Pombe Magufuli kuonyesha nia ya kuwasaidia wananchi waliojenga kiholea katika maeneo mbalimbali nchini kwa kurasimisha maeneo lakini bado wananchi wa Bukoba hawajaona umuhimu huo na wengi hawajitokezi kuchangamkia hati za ardhi.

‘’Tatizo bado liko kwa wananchi, bado hawajajitambua kwa sababu kitendo cha kurasimisha maeneo lakini wananchi mnashindwa kuchangia fedha kwa ajili ya kupangwa, kupimiwa na hatimaye kumilikishwa ardhi, nia ya serikali ni kuwamilikisha wananchi,’’ amesema Mabula.

Aidha, amesema kuwa zoezi la kurasimisha maeneo siyo endelevu na lengo ni kubwa ni kuwawezesha wananchi kiuchumi na kubainisha kuwa pale mwananchi atakapopewa hati itamsaidia kupata mkopo na kujikwamua kiuchumi.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameipongeza halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kwa kuweza kupima jumla ya viwanja 11,330 katika zoezi la urasimishaji na kueleza kuwa hali hiyo inaonesha jinsi makampuni yaliyoshiriki katika zoezi hilo yalivyokuwa makini katika kazi zake.

Mapema akipokea taarifa za idara za ardhi katika halmashauri ya Manispaa ya Bukoba na halmashauri ya Bukoba Vijijini, NaibuWaziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameonesha kutoridhishwa na kasi ya ukusanyaji mapato ya serikali kupitia sekta ya ardhi katika halmashauri hizo mbili ambazo zote hakuna hata moja iliyofikia asilimia hamsini ya malengo katika kipindi cha mwaka 2018/2019.

Katika taarifa yake iliyosomwa na Mkuu wa Idara ya Ardhi, Catres Rwegasira Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba imekusanya shilingi milioni 228.512 kati ya milioni700 ilizopangiwa huku ile ya Bukoba Vijijini iliyosomwa na Kaimu Mkuu wa Idara John Mwingira ikikusanya milioni 29.61 kati ya milioni 200 ilizopangiwa kukusanya katika kipindi cha mwaka 2018/2019.

 

 

Profesa Lipumba ashinda uenyekiti CUF kwa kishindo
Wanafunzi 397 kidato cha kwanza wilayani Wanging'ombe hawajaripoti shuleni