Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Slovenia, Tanja Fajon na ujumbe wake amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatuikilenga kuimarisha na kukuza uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na Slovenia sambamba na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano.
Waziri Fajon katika siku yake ya kwanza nchini amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax jijini Dodoma, ambapo mazunguzo yao yalijikita kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kuanisha maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Slovenia.
Mazungumzo hayo pia yalihusisha uandaaji wa mazingira na utaratibu wa kusainiwa kwa Hati za Makubaliano katika maeno mapya ya ushirikiano yaliyoainishwa ambapo maeno mapya ya ushirikiano yaliyoibuliwa wakati wa mazungumzo hayo ni uzalishaji dawa, usimamizi wa rasilimali maji, utunzaji wa mazingira, ulinzi na usalama, uchumi wa buluu, sayansi na teknolojia, kilimo, Elimu,biashara na uwekezaji.
Aidha, Waziri Dkt. Tax pia alitumia fursa hiyo kumweleza Waziri Fajon kuhusu juhudi zilizochukuliwa na Serikali na mafanikio yaliyopatikana nchini kutokana na juhudi hizo ikiwemo kupatikana kwa maridhiano ya kisiasa, kuimarika kwa Demokrasia, Haki za Banadamu, uhuru wa vyombo vya habari na uzingatiwaji wa usawa wa jinsia katika maendeleo.
Kwa upande wake Waziri Fajon, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika kuboresha mazingira ya Demokrasia na Utawala Bora nchini sambamba na kuendelea kusimamia vyema maendeleo ya uchumi licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali duniani zinazo dhoofisha ustawi wa uchumi.
Ziara hiyo ni muendelezo wa matokeo ya juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Mataifa mengine duniani na Waziri Fajon pia anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Viongozi mbalimbali wa Serikali.