Serikali imewatoa wasiwasi Watanzania kuhusu hali ya chakula nchini na kueleza kuwa kuna ziada ya chakula zaidi ya asilimia 123 ikilichozalishwa msimu uliopita.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Tate Ole Nasha alipokuwa akizindua tovuti ya Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) leo mjini Dodoma.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema kuwa hali ya chakula nchini inaridhisha ambapo tafsiri ya hali ya chakula inatokana na ukweli kuwa uzalishaji wa chakula kwa asilimia 100 inaonesha kuna chakula, asilimia 101 hadi 120 kuna utoshelevu wa chakula na asilimia zaidi ya 120 hali hiyo inatafsiriwa kuwa kuna chakula cha kutosha kwa miaka mitatu hadi minne.

“Nawasihi Watanzania kutunza chakula kilichopo ili kitumike sasa na baadae, hali ya uwepo wa chakula ndani ya nchi itaonesha kuwa kuna usalama kwa wananchi na wanaweza kuendelea na shughuli zao za kila siku” alisema Naibu Waziri huyo.

Aidha, Naibu Waziri Ole Nasha amewatahadharisha Watanzania kutunza chakula kutokana na nchi jirani kutokuwa na hali nzuri ya upatikanaji wa chakula ambapo katika nchi 15 za SADC, kati ya hizo nchi 13 hazina chakula za kutosha.

Kuhusu tovuti aliyoizundua, Naibu Waziri Ole Nasha amesema kuwa tovuti hiyo itatoa taarifa zinazokwenda na wakati badala ya kutumika kama maktaba ya kutunzia kumbukumbu za Serikali na iwe na uwezo wa kuwashirikisha wasomaji ili kupata mrejesho kutoka kwa wasomaji ambao utasaidia kufanya maboresho katika utendaji na kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake Msemaji wa Serikali Hassan Abbas amesema kuwa kwa sasa mawasiliano ya haraka duniani yamehamia kwenye mitandao ya kijamii, kwa muktadha huo, Serikali imeanza kuwasiliana na wananchi kwa haraka kwa kutoa taarifa mbalimbali kwa wakati kwa njia ya mitandao ya kijamii badala ya kusubiri vyanzo vingine vya habari.

Akitolea mfano Msemaji huyo amesema kuwa dunia ina takribani watu wapatao trilioni saba ambapo zaidi ya watu trilioni tatu wanatumia mitandao ya kijamii na asilimia 91 ya makampuni yote duniani wanatumia mitandao ya kijamii zaidi ya miwili hadi mitatu.

Awali akimkaribisha Nibu Waziri, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA amesema kuwa kuanzishwa kwa tovuti hiyo itawasaidia wananchi kupata huduma mahali walipo bila kutembelea ofisi husika au kuonana na mtoa huduma.

Tovuti iliyozinduliwa leo ni www.nfra.go.tz, yenye lengo la kurahisisha utoaji taarifa za taasisi hiyo kwa wananchi

Waziri Lukuvi Awasilisha Mswaada Wa Sheria ya Uthamini, Usajili na Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Nchini
Serikali Yaadhimisha Siku Ya Kisomo Duniani, Lengo Kubwa ni Kuhakikisha Kila Mtanzania Anaelimika