Wakati Ihefu FC ikikosa mchezaji kwenye mbio za kuwania ufungaji bora ligi hadi sasa, benchi la ufundi limesema tatizo ni ufinyu wa namba, huku likikiri ugumu wa kupata kikosi cha kwanza.

Ihefu FC licha ya mwenendo mzuri ilionao kwenye ligi kuu kwa sasa, lakini haina mchezaji aliye kwenye vita ya ufungaji bora ambapo kinara wao wa mabao, Raphael Daudi Loth’ ametupia matano tu, huku Jafar Kibaya akiwa na manne.

Kwa sasa Mshambuliaji wa Young Africans, Fiston Mayele ndiye kinara wa mabao akiwa amefunga 16, huku Moses Phiri na Saido Ntibazonkiza wa Simba SC wakifuata kwa mabao 10 kila mmoja.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Zuber Katwila amesema kukosekana kwa wachezaji wao kwenye orodha ya wafungaji vinara ligi kuu ni kutokana na ufinyu wa namba kwani hakuna mwenye uhakika wa kucheza dakika 90.

Amesema mbali na vita ya nafasi kikosini hata benchi la ufundi hukuna sana kichwa kuamua nani aanze au kusubiri benchi kutokana na kila mmoja kuwa na uwezo binafsi.

“Kwanza tulikuwa na mkakati wa kuipambania timu kutafuta matokeo, kwa hiyo unakuta hakuna mwenye uhakika wa namba kwa sababu kila anayecheza anaweza asimalize dakika 90,”

“Hata benchi la ufundi tunatumia nguvu na akili nyingi kupata kikosi cha kwanza, mfano sehemu ya mbele tuna mastaa nane utamuanzisha nani na umuache yupi benchi,” amehoji Katwila.

Kuhusu kupoteza mechi tatu mfululizo ikiwamo moja ya Kombe la Shirikisho (ASFC), Katwila amesema matokeo ya mpira licha yao kuamini watashinda zote na kwamba kwa sasa wanajiandaa kutopoteza tena kati ya zilizobaki.

“Lengo ilikuwa ni kushinda mechi zote lakini mpira una matokeo yake na sasa tunaendelea kujipanga na michezo mitatu iliyobaki kumaliza nafasi nzuri,” amesema kocha huyo mzawa

Serikali yajipanga upitiaji Takwimu za Sensa uchumi, kijamii
Biashara Tanzania, Ufaransa inakua - Dkt Tax