Uongozi Namungo FC umeeleza kuwa kwa sasa hawana mpango wa kutafuta kocha mpya, wakimpa nafasi zaidi aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo, Denis Kitambi.
Kauli hiyo imeibuka baada ya Kitambi kuiongoza timu hiyo katika mechi mbili na kupata ushindi dhidi ya Azam wa mabao 3-1 na sare dhidi va Coastal Union tangu arithi mikoba ya Cedric Kaze.
Ofisa Habari wa Namungo, Kindamba Namlia amesema uongozi haujaamua chochote kuhusu kuhitaji kocha mpya na sasa inaendelea na Kitambi mpaka itakapoamua vingine siku za usoni.
“Mpaka sasa hakuna mipango mipya juu ya kocha mpya yaani uongozi unaendelea na Kitambi kwa sasa, hiyo ndio kauli rasmi mpaka hapo baadae kama kutakuwa na mabadiliko yoyote tutaweka wazi lakini kwa sasa hicho ndicho kilichopo,” amesema Namlia.
Kaze raia wa Burundi alitangaza kujiuzulu katika timu hiyo baada ya kuiongoza katika mechi sita za awali msimu huu bila ushindi wowote ambapo aliambulia sare tatu na kufung wa mechi tatu pia.