Uongozi wa Namungo FC unaamini kikosi chao kilikuwa na nafasi ya kufanya vizuri katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23, lakini kitendo cha kukamiwa na timu pinzani zinazoshiriki Ligi hiyo kimewaponza.
Kwa sasa Namungo FC inashika nafasi ya sita kwenye Msimamao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na alama 35, imecheza michezo 26 huku Young Africans ikiongoza ikiwa na alama 68 ikifuatiwa na Simba yenye alama 63.
Mwenyekiti wa Namungo FC Hassan Zidadu amesema anaamini changamoto ta kukamiwa na timu pinzani za ligi kuu, kutokana na ushiriki wao Kimataifa misimu miwili iliyooita umechangia hali hiyo.
Namungo FC ilishiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu wa 2020/21 na kushika nafasi ya mwisho kwenye Msimamo wa Kundi D lililokuwa na Raja Casablanca, Pyramids na Nkana.
Zidadu ambaye ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini amesema msimu huu wameshindwa kufanya vizuri lakini watakaa chini na kuja na mipango ya kuhakikisha wanafanya vizuri msimu ujao.
“Tulijisahau kutoka na ule ushiriki wetu wa mashindano ya Kimataifa, timu zimetuchukulia kama sisi ni wakubwa, lakini sisi wenye tunajiona wa kawaida, hapo ndipo tulipoteleza, wenzetu wanajitoa kwamba sisi ni timu kubwa lakini vijana wetu hawalielewi hilo.”
“Kwetu sisi tunachukulia kama ni somo kwahiyo msimu ujao tutaenda kukaa chini ili kuelekezana kwamba kila mechi kwetu iwe kama fainali,” alisema Mwenyekiti huyo.”
Mwenyekiti huyo amewataka mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na wasiwasi kwani wanaweka mikakati ya kuhakikisha msimu ujao wanafanya vyema na kufuzu kucheza mashindano ya kimataifa.