Kocha Mkuu wa Young Africans Nesreddine Nabi amewaangalia wapinzani wake Namungo FC na kusema wanahitaji kujiweka fiti zaidi kuhakikisha wanafanikiwa kupata alama tatu katika mchezo dhidi yao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Young Africans itacheza dhidi ya Namungo FC Aprili 23, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kocha huyio kutoka nchini Tunisia amesema katika mchezo wa kwanza walitoka sare ya 1-1 wakiwa ugenini, ana imani watakuwa wamebadilika kwa sababu wamefanya mabadiliko Benchi la Ufundi na kuwa na kiwango bora zaidi.

“Namungo FC ina wachezaji wazuri ukiangalia Benchi la Ufundi tofauti na mchezo wa kwanza, tunatakiwa kujiandaa kuhakikisha tunafikia malengo yetu ya kupata pointi muhimu katika michezo iliyopo mbele yetu,” amesema Nabi na aliongeza.

“Kazi kubwa kwa sasa kuendelea ni kujiimarisha zaidi kila nafasi ukiangalia katika mechi iliyopita kuna baadhi ya wachezaji akiwemo Saido Ntibanzokiza na Fiston Mayele kucheza wakiwa wagonjwa.”

Amesema baada ya mapumziko ya siku chache timu imerejea kambini ameona nyota hao na baadhi ya majeruhi kurejea uwanjani na matumaini makubwa ya mechi ijayo kuwa na kikosi kipana.

Nabi amesema kazi kubwa anayoifanya kwa sasa anaendelea kuisuka safu ya ushambuliaji kuwa imara na kurejea ilivyo awali kushinda kila mechi katika ligi hiyo.

Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kumiliki alama 51, ikifuatiwa na Mabingwa Watetezi Simba SC wenye alama 41.

Kocha Pablo: Wachezaji nimewapa elimu ya VAR
Erasro Nyoni afichua mzuka wa Simba SC