Mabingwa mara nane mfululizo wa Ligi ya soka Ujerumani Bundesliga, Bayern Munich kesho Jumamosi watashuka dimbani kumenyana na Bayer 04 Leverkusen katika mchezo wa fainali kombe la shirikisho (DFB Pokal).
Bayern Munich walifanikiwa kutwaa taji la Bundesliga msimu huu majuma mawili yaliyopita, na sasa wanahitaji taji la pili nchini Ujerumani, lakini hawatokua na namna nyingine zaidi ya kupambana ndani ya dakika 90 hiyo kesho.
Hata hivyo mabingwa hao wanatarajia upinzani wa dhati kutoka kwa Bayer 04 Leverkusen ambao wanahitaji kuweka heshima msimu huu, kwani hawajaonja mafanikio tangu mwaka 1993 licha ya kunyemelea kwa karibu kulitwaa taji la Bundesliga takriban mara nane, kombe la DFB Pokal pamoja na ligi ya mabingwa barani Ulaya.
“Tutaendelea kuwa na njaa,” alisema mchezaji wa Bayern, Joshua Kimmich, baada ya kufanikiwa kulitwaa taji la Bundesliga. Bayern walipoteza fainali ya kombe la shirikisho 2018 dhidi ya Eintracht Frankfurt.
Matumaini ya kurudia tena kushinda mataji matatu kama 2013 bado yapo huku ligi ya mabingwa wa Ulaya ikitarajiwa kurejea tena mwezi ujao.
FC Bayern Munich wanakaribia kufuzu katika robo fainali, baada ya kushinda mechi yao ya ugenini dhidi ya chelsea kwa idadi ya kutosha ya mabao.