Wakata Miwa kutoka Manungu, Turiani mkoani Morogoro (Mtibwa Sugar), wamejinasibu kuendelea kupambana kuhakikisha kikosi chao kinasalia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao (2020/21).

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Habari wa Mtibwa, Thobiasi Kifaru baada ya kikosi hicho kuwa katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na jumla ya alama 37 wakicheza michezo 32, huku wakisaliwa na mechi sita tu, ambazo wanatakiwa kupata ushindi ili kuendelea kubaki katika ligi hiyo.

Akizungumza kutoka Morogoro, Kifaru alikiri kikosi hicho kupitia katika mazingira magumu ndani ya msimu huu unaolekea ukingoni kwa kushika nafasi, ambayo hawajaizoea kuikalia, kama ilivyosasa.

“Nakiri ni msimu mgumu kwetu ambao umetufanya kubaki kwenye mazingira magumu ambayo hatujawahi kushika kwenye msimamo wa Ligi tangu tumepanda kwa kushika nafasi ya 13 kwenye msimamo hatuwezi kukata tamaa, bado tuna michezo sita ya kupigania tubaki, alisema Kifaru.”

Alisema katika kipindi hiki, benchi la ufundi kwa kushirikiana na viongozi wengine bado wanaendelea kutimiza majukumu yao kwa kuhakikisha vijana wa kikosi hicho wanaandaliwa kiushindani kwa michezo iliyobaki ili kupata ushindi kwa mechi zilizosalia.

Alisema licha ya kwamba wanacheza michezo hiyo, huku Simba ikiwa tayari imeshachukua ubingwa, lakini wao bado wanapresha kubwa ya kupambana kusaka pointi muhimu za kuepuka kushuka daraja msimu huu wa mwaka 2019/2020.

Azam FC yawataja Mkude, Chama, Fraga
Nani kutwaa DFB Pokal 2020?