Viungo Mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC Jonas Mkude, Clatous Chama na Gerson Fraga wametajwa kama sumu ya kuvuruga mipango ya Azam FC, wakati wa mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho uliochezwa juzi Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es salaam.

Simba SC walishinda mabao mawili kwa sifuri na kutinga hatua ya Nusu Fainali, watakutana na watani zao wa jadi Young Africans Julai 12 Uwanja wa Taifa, Dar es salaam.

Siri ya viungo hao watatu kuvuruga mipango ya Azam FC, imefichuliwa na kocha msaidizi wa klabu hiyo yenye maskani yake makuu Chamazi Complex, Dar es salaam Vivier Bahati.

Akizungumzia mchezo huo, kocha Bahati, amesema Simba SC walikuwa bora katika safu ya kiungo na nyota hao walikuwa kikwazo kikubwa kwa timu yao.

“Simba walikuwa bora katikati, ndio sehemu imecheza mpira mwingi sana, hadi kuharibu mipango yetu na kushindwa kufanya vizuri katika mchezo huo wa robo fainali,” alisema Bahati.

Amesema kikosi chao kilijiandaa vizuri kuelekea mchezo huo wa Robo Fainali, huku wakiwaonyesha wachezaji wao ubora na mapungufu ya Simba ili kuweza kuyatumia na kupata matokeo mazuri.

“Tuliandaa mipango vizuri lakini ubora wa viungo wa Simba, waliharibu mipango yetu, yale ambayo tuliyapanga hatukuyaona kabisa pale uwanjani kwa wachezaji wetu, walistahili ushindi,” Bahati alisema.

Ameongeza baada ya kuondolewa kwenye michuano hiyo, sasa wanajipanga kuhakikisha wanalinda heshima kwa kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Sahare All Stars: Tutafanya maajabu ASFC
Kifaru: Tuna michezo sita ya kupigania kubaki Ligi Kuu