Uongozi wa Young Africans umetoa neno la Shukurani kwa Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo, kufuatia ushindi wa 2-0 walioupata jana Jumapili (April 23) dhidi ya Mabingwa wa Nigeria Rivers United.
Young Africans ilicheza ugenini nchini Nigeria mchezo wa Mkondo wa Kwanza, huku mabao ya ushindi yakifungwa na Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Mayele.
Neno la Shukurani kwa Mashabiki na Wanachama limetolewa katika kurasa za Mitandao ya Kijamii za Young Africans, lakini wameombwa kuendelea kushikamana kwa pamoja ili kufanikisha matokeo mazuri katika mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Jumapili (April 30) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Taarifa ya neno la shukurani: “Shukrani kwa Wanachama, Mashabiki na Wapenzi wa Young Africans SC kwa maombi na sapoti yenu mnayotupa wakati wote.”
“Kazi bado haijaisha kwenye mchezo wetu wa kwanza wa robo fainali #cafcc dhidi ya Rivers United, bado tuna mchezo wa pili na tunawaomba #wananchi wote kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa tarehe 30.04.2023 kwenye mchezo wetu wa pili muhimu na wa kihistoria.”
Katika mchezo wa Mkondo wa Pili, Young Africans itapaswa kulinda ushindi wake wa 2-0 ama kusaka ushindi zaidi, lakini wageni wao Rivers United watatakiwa kusaka ushindi wa mabao 3-0 ili kujihakikishia nafasi ya kutinga Nusu Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu wa 2022/23.