Ikiwa leo ni siku ya pili tangu ilipotolewa taarifa kuwa msanii Roma Mkatoliki alitekwa na watu wasiojulikana akiwa pamoja na Moni Centrozone, mtayarishaji wa muziki wa Tongwe Records, Bin Laden katika studio za Tongwe Records, Waziri wa zamani wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amemlilia msanii huyo.

Nape emetoa kilio chake kupitia ukurasa wake wa Twitter, akitumia maneno matatu pekee yanayosomeka kwa hisia za ndani kuwa ni mtu anayemlilia mpendwa wake.

“Roma! Oooooh No!” ametweet Nape.


Mbunge huyo wa Mtama ameongeza nguvu kwa kilio cha wadau wa muziki pamoja na wasanii waliotumia mitandao ya kijamii kushinikiza ifahamike alipo msanii huyo na wenzake.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa jana na uongozi wa Tongwe Records, watekaji walifika katika studio hizo na kuwahoji waliokuwepo, kisha kuondoka nao wote pamoja na baadhi ya vifaa vinavyotumika kurekodia muziki, kwenda kusikojulikana.

Mke wa Roma, Nancy ameeleza kuwa alifika katika vituo kadhaa vya polisi jijini Dar es Salaam kuulizia taarifa za mumewe, lakini alielezwa kuwa taarifa za Roma hazikuwepo.

Akizungumza kwa uchungu kwenye vyombo mbalimbali vya habari, Nancy aliwaomba Watanzania kwa ujumla pamoja na vyombo vya usalama kusaidia kufahamu alipo mumewe.

“Serikali, waandishi wa habari, Watanzania, yeyote aliyeona, aliyesikia, anayeweza kutusaidia Roma yuko wapi naombeni msaada wenu,” alisema.

Leo mchana, wasanii wamekutana katika studio za Tongwe Records kwa lengo la kuzungumzia suala hilo zito ambalo limevunja mioyo ya wadau wa muziki, familia na ndugu wa Roma na wenzake.

 

 

 

 

Wadau wa michezo wapewa siri ya mafanikio, watakiwa kuijtokeza
Sirro afunguka kuhusu kupotea kwa Roma, kesho kutoa taarifa kamili