Wadau wa michezo hapa nchini wameombwa kujitokeza ili kuweza kudhamini michezo ya wanawake ili itambulike na kupata mafanikio ya ndani na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Prof. Elisante Ole Gabriel leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa anazindua Kongamano la wanawake na Michezo liliondaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Amesema kuwa michezo inahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wadhamini  hivyo ni wajibu kwa wadhamini mbalimbali kuona jitihada zinazoonyeshwa na wanawake hao na amewaomba waziunge mkono.

“Nawaomba wadhamini mjitokeze kuunga mkono jitihada hizi za wanawake ili zilete mafanikio katika michezo ya wanawake,” Amesema Prof  Elisante.

Kwa upande wake, Jenifer Mmasi ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa amesema kuwa kongamano hilo lina lengo la kuwakutanisha wanawake ambao ni wanamichezo kupata ujuzi na namna bora ya kutumia michezo katika jamii zao kama njia ya kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo.

Hata hivyo, Kongamano hilo la siku moja linalenga kujadili jinsi wanawake wanavyoweza kufanikiwa kupitia michezo pamoja na changamoto ambazo wanawake wanakutana nazo katika kushiriki michezo  na kuzitafutia  ufumbuzi

Majaliwa atoa ujumbe mzito kwa Watanzania
Nape Amlilia Roma Mkatoliki, 'Ooooooh No!'