Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amesema kikosi chake kitatakiwa kucheza kwa nidhamu kubwa dhidi ya Mbeya Kwanza FC, ili kufanikisha lengo la kupata ushindi utakaowasogeza kwenye Ubingwa msimu huu.
Young Africans itacheza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kesho Ijumaa (Mei 20), ikihitaji kushida mchezo huo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuupoka ubingwa kutoka kwa Watani zao Simba SC.
Kocha Nabi akiwa katika Mkutano na Waandishi wa Habari leo Alhamis (Mei 19) jijini Dar es salaam, amesema wanakwenda kucheza dhidi ya timu inayoburuza mkia kwenye msimamo, hivyo anajua haitakua kazi rahisi kwa kikosi chake kupata ushindi zaidi ya kupambana maradufu.
Amesema siku zote katika Ligi, timu zinazoshika nafasi ya mwisho huwa zinakua na nguvu ya ajabu kwenye michezo yao ya mwisho, hivyo ni wajibu wa kila mchezaji atakayempa nafasi kesho Ijumaa (Mei 20) kupambana na kufikia malengo waliojiwekea.
“Timu ambazo ziko chini ndio zinazosumbua sababu hili liliitokeza kwenye mechi na Prisons kwa hiyo inatuhitaji tuwe makini zaidi kupata ushindi mechi ya kesho na Mbeya Kwanza FC.”
“Sio katika Ligi ya hapa Tanzania pekee, hata kwingineko Dunia, timu zinazokamata nafasi za chini kwenye msimamo huwa na mtazamo mkubwa wa kupambana ili kuepuka kushuka Daraja, itatulazimu kupambana sana kesho ili tusirudie makosa.” amesema Kocha Nabi.
Young Africcans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 60, huku ikihitaji alama 09 kujitangazia Ubingwa msimu huu, baada ya Simba SC kupata sare ya 1-1 dhidi ya Azam FC jana Jumatano (Mei 18).
Mbeya Kwanza FC inaburuza mkia wa Msimamo wa Ligi Kuu hadi sasa, ikiwa na alama 21, hivyo itahitaji kupambana vilivyo dhidi ya Young Africans ili kujinasua kwenye nafasi hiyo.