Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi, amenasa siri za Rivers United ya Nigeria baada ya kushirikiana na wataalamu wengine katika benchi lake la ufundi.

Young Africans watakuwa wageni wa Rivers United ya Nigeria, keshokutwa Jumapili (April 23) katika mchezo wa kwanza wa hatua ya Robo Fainali ya michunao ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC), ambao utachezwa kuanzia saa 10.00 jioni katika Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabio mjini Uyo.

Katika mazoezi waliyofanya jana jioni mjini Lagos, Nigeria, Kocha Nabi alianza kwa kuangalia ubora na mapungufu yao kuhakikisha wanapata matokeo katika uwanja wa ugenini.

Ameongeza kuwa hivi sasa hana kazi kubwa zaidi ya kuendelea kuwapa majukumu safu yake ya ushambuliaji inayoongozwa na Fiston  Mayele na Kennedy Musonda na kuwataka kuongeza umakini.

“Najua Rivers wana walinzi wazuri, sisi tutafanya kazi ya kushambulia kwa kushtukiza kuhakikisha tunawashangaza wenyeji wetu,” amesema.

Amesema anaimani kubwa na vijana wake kumpa matokeo mazuri katika mchezo huo wa ugenini kabla ya kurejea nyumbani.

“Kikubwa ni kuendelea kuwapa mbinu wachezaji wetu tunazungumza nao kwa kuwaambia akili zao sasa ni mechi ijayo dhidi ya Rivers, hatutakiwi kuwaza kitu kingine, tunaenda kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu,” amesema.

Aliongeza kuwa wachezaji wake ni bora na wanaweza kufanya vizuri katika mechi zijazo na kuwapa matokeo chanya katika dakika 180 dhidi ya Rivers United.

Kikosi cha Young Africans kilitua jana Alhamis (April 20) mchana mjini Lagos, Nigeria na kufanya mazoezi ya jioni kabla ya leo Ijumaa (April 21) kutakiwa kwenda mji wa Uyo ambapo mchezo huo utachezwa.

Kikosi cha Yanga kilitinga hatua ya Robo Fainali ya CAFCC baada ya kuongoza Kundi D kwa kufikisha pointi 13 ilizovuna katika michezo sita. Imeshinda michezo minne, imepoteza na kutoka sare mchezo mmoja mmoja.

Wachezaji 23 wa Yanga waliopo Nigeria ni Djigui Diarra, Metacha Mnata, Erick Johola, Ibrahim Abdallah, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Yannick Bangala, Khalid Aucho, Jesus Moloko, Joyce Lomalisa, Shomary Kibwana na Farid Mussa.

Wengine ni Salum Abubakar, Zawadi Mauya, Djuma Shaaban, Mudathir Yahya, Kennedy Musonda, Fiston Mayele, Clement Mzize, Mamadou Doumbia, Tuisila Kisinda, Benard Morrison na Stephen Aziz Ki.

Gabriel Geay afichua siri Boston Marathon 2023
Waliotambika makaburini kulinda penzi wadakwa na Polisi