Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Nabi ameapa kupabana Kufa na Kupona ili kuingamiza TP Mazembe katika Uwanja wake wa nyumbani mjini Lubumbashi.
Young Africans itakua mgeni wa TP Mazembe mapema mwezi April kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa Kundi D Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku ikikumbuka ushindi wa 3-1 iliyoupata dhidi ya miamba hiyo ya DR Congo ilipocheza Uwanja wa Benjamin Mkapa mwezi uliopita.
Nabi amesema mchezo huo una umuhimu mkubwa sana kwa Young Africans ambayo ina lengo la kumaliza kinara wa Kundi D, na kuweka Rekodi mpya katika historia ya Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na CAF.
Amesema kama kikosi chake kitaibuka na ushindi ugenini dhidi ya TP Mazembe kitajihakikishia kuwa kinara wa Kundi D, na kupata ahuweni ya kukutana na timu zitakazomaliza nafasi ya pili katika Kundi A, B na C.
“Sote tunafahamu kuwa kama tukimaliza nafasi ya kwanza kuna faida ya kukutana na timu za pili katika makundi mengine, lakini kama tukishindwa kupata nafasi hiyo tunaweza kuangukia kwa timu ambazo zimefanya vizuri kwenye hiyo michezo sita,”
“Haitakuwa rahisi lakini mimi sio kocha rahisi wa kukata tamaa napenda kuishi kwa malengo nadhani kitu bora ni kujipanga na kucheza kwa hesabu sahihi.” amesema Nabi
Young Africans inaongoza msimamo wa Kundi D ikiwa na alama 10 sawa na US Monastir ya Tunisia yenye tofauti ndogo ya mabao ya kufunga na kufungwa, huku AS Real Bamako ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 05.
TP Mazembe ambayo tayari imeshatupwa nje ya michuano hiyo inaburuza mkia ikiwa na alama 05, hivyo mchezo dhidi ya Young Africans itautumia kama sehemu ya kuweka heshima kwenye Uwanja wake wa nyumbani mjini Lubumbashi.