Rais wa Klabu Bingwa nchini Ufaransa Paris Saint-Germain, Nasser Al-Khelaifi amekanusha madai ya nahodha wa Argentina, Lionel Messi aliyesema klabu hiyo haikumpa pongezi baada ya kuliongoza taifa lake kushinda Kombe la Dunia mwaka jana.

Messi alifunga mara mbili kwenye mchezo wa fainali na kufunga penalti yake ambapo Argentina walinyakua kombe hilo kwa kuwafunga Ufaransa kwa matuta na hilo kuwa taji la tatu kwa taifa lake.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 36, ambaye aliondoka PSG baada ya mkataba wake na klabu hiyo kumalizika Juni mwaka huu, alisema: “Nilikuwa mchezaji pekee kwenye kikosi cha wachezaji 25 kilichoshinda Kombe la Dunia na Argentina ambaye sikupongezwa na klabu yangu.

“Inafahamika…. kwa sababu yetu sisi Argentina, Ufaransa ilishindwa kutetea Kombe la Dunia.”

Hata hivyo, Al-Khalaifi alikana kwa kusema: “Kama kila mtu alivyoona, kwa sababu tulichukua hadi video, tukimpongeza Messi kwenye mazoezi lakini pia tulimpongeza binafsi,” alisema Al-Khalaifi alipozungumza na waandishi wa habari.

“Lakini kwa heshima, sisi ni klabu ya Ufaransa. Tulipaswa kuwa makini kumpongeza uwanjani. Lazima tuiheshimu nchi aliyoishinda, wachezaji wenzake kwenye klabu wanaocheza timu ya taifa ya Ufaransa na mashabiki wetu vilevile.”

Nyota huyo wa Argentina alijiunga na klabu ya Marekani Julai mwaka huu na kushinda taji lake la kwanza la ligi na timu hiyo Agosti.

Mwakinyo abadilishiwa mpinzani
JKT Tanzania kuanza na Kagera Sugar Shinyanga