Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg ameonya kuwa vita ya Urusi nchini Ukraine inaweza kuendelea kwa miaka mingi na mataifa ya magharibi hayapaswi kurudi nyuma katika kuisaidia Ukraine.
Kwa mujibu wa Gazeti la Bild am Sonntag la nchini Ujerumani, katika mahojiano Stoltenberg amesema nchi za Jumuiya ya NATO ni lazima zijitayarishe na ukweli kuwa vita nchini Ukraine inaweza kudumu kwa muda mrefu na ni muhimu kuendelea kuipatia msaada Ukraine.
Amesema kwamba kuipatia Ukraine msaada wa silaha mamboleo kutatanua nafasi ya vikosi vya nchi hiyo kulikomboa jimbo la mashariki la Donbas ambalo limeangukia mikononi mwa Urusi.
Kiongozi huyo pia amesema mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya NATO utakaofanyika mjini Madrid baadae mwezi huu, unatarajiwa kufikia makubaliano ya kuisaidia Ukraine kuboresha zana zake za vita na kuachana na zile za enzi ya dola ya kisovieti.