Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Februari 2021 umepungua kutoka asilimia 3.5 kwa mwaka ulioishia Januari 2021 hadi kufikia asilimia 3.3.
Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Taifa NBS, Ruth Minja ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa mfumuko wa bei katika kipindi hicho.
Minja amesema hiyo inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Februari 2021, imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia Januari mwaka huu.
Amezitaja baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizopungua bei katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na samani kwa asilimia 5.3, mafuta ya taa kwa asilimia 15.7, vifaa vya nyumbani kama pasi ya umeme kwa asilimia 4.7, vyombo vya ndani kwa asilimia 3.3, dizeli asilimia 22.8 na petroli kwa asilimia 13.4.
Minja amesema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Februari mwaka huu umeongezeka kutoka asilimia 2.8 Januari 2020 hadi kufikia asilimia 3.6.