CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimetangaza kutoshiriki Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Muhambwe mkoani Kigoma, kwa maelezo kwamba dosari zilizojitokeza katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2020, hazijafanyiwa kazi.
Hatua hiyo imetangazwa leo ljumaa tarehe 2 Aprili 2021, na Mkuu wa ldara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye, wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.
Simbeye amesema kuwa, mapendekezo waliyotoa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, hayajafanyiwa kazi, hivyo chama hicho hakina imani kushiriki kwenye uchaguzi wa Muhambwe, kwa kuwa chombo kinachousimamia (NEC), haikijafanyiwa mabadiliko.
“Baada ya uchaguzi wa 2020, tulisema NCCR tunahitaji muafaka wa kitaifa, tuliishauri Serikali kwamba ni vyema muafaka wa kitaifa ukapatikana sababu utaamua hatma ya Taifa letu juu ya kitu kinachoitwa katiba mpya, tume huru na maridhiano ya kisiasa na kiuchumi,” amesema Simbeye.
Hivi vyote havijafanyika tena, upinzani hawajakaa kuzungumza kinachohusu hatma ya Watanzania, maendeleo na siasa ya Kitanzania, tunaendaje kwenye uchaguzi tukiwa katika hali hii?” amehoji Simbeye.
Uchaguzi mdogo katika Jimbo la Muhambwe umeitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), baada ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo (CCM), Atashasta Nditiye, kufariki dunia tarehe 12 Februari 2021.