Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa ombi kwa nchi za ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kushirikiana kwa pamoja katika kuendeleza jitihada za kuwainua na kuwawezesha wanawake kwenye nchi zao.
Amesema hayo akiwa katika mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Bingu uliopo Jijini Lilongwe nchini Malawi.
“Nataka kuwasihi kaka zangu wa ukanda huu tuendelee kushirikiana katika kuendeleza jitihada za kuwainua na kuwawezesha kiuchumi na kisiasa wanawake kwenye nchi zetu,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameomba jitihada za upatikanaji wa chanjo kwa ajili ya Uviko-19 kuendelezwa kwani mahitaji ya chanjo ni makubwa.
“Mahitaji ya chanjo bado ni makubwa na hatuna budi kuendelea kuongeza jitihada za upatikanaji wa chanjo na pia kuzishawishi kampuni zinazozalisha chanjo kuridhia kutoa vibali vya teknolojia, ili kuruhusu chanjo ziweze kuzalishwa sehemu nyingine,“ amesema Rais Samia.