Kocha mkuu wa Young Africans, Cedric Kaze amesema kikosi chake kitawakosa baadhi ya wachezaji kwenye mchezo wa leo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union.
Young Africans watakua ugenini Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga, kucheza mchezo wa mzunguuko wa 22 wa Ligi Kuu, huku wakiongoza msimamo wa ligi hiyo kwa kumiliki alama 49.
Kocha Kaze amesema mshambuliaji Ditram Nchimbi ni miongoni mwa nyota ambao wataukosa mchezo dhidi ya Coastal Union, baada ya kupata majeraha kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Ken Gold.
Mbali na Nchimbi mwenye pasi mbili za mabao kati ya 34 yaliyofungwa na Young Africans, Kaze amemtaja beki wa kushoto Adeyum Saleh ambaye yupo kwenye orodha ya wachezaji walio majeruhi.
Mwingine ni mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saido Ntibanzokiza na kiungo Balama Mapinduzi ambao bado hawajarejea Kwenye ubora huku Carlos Carlinhos akikabiliwa na adhabu ya kadi nyekundu aliyopata kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Ken Gold.
Wakati Young Africans ikijiandaa kuelekea kwenye dimba la CCM Mkwakwani huku wakiongoza msimamo wa Ligi Kuu, wenyeji wao Coastal Union wapo nafasi ya nafasi ya 13 na alama zake ni 23.