Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kimewasili salama mjini Istanbul, Uturuki ambako kitaweka kambi ya siku tano kabla ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2021), dhidi ya Tunisia Novemba 13.
Mchezo huo wa kundi J utachezwa mjini Tunis, huku Stars ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita wa kundi hilo kwa kufungwa na Libya mabao mawili kwa moja, huku ikishinka nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 3.
Stars iliifunga Equatorial Guinea mabao mawili kwa moja, kwenye mchezo wa kwanza wa kundi hilo uliochezwa Dar es salaam Novemba mwaka 2019.
Kocha mkuu wa Stars Ettiene Ndayiragije amesema kikosi chake kipo tayari kwa maandalizi ya siku kadhaa nchini Uturuki, na ana matumaini makubwa ya kufanya vyema mbele ya Tunisia ambao wanaongoza msimamo wa kundi J, kwa kufikisha alama 6.
Amesema amewafuatilia Tunisia na kubaini mbinu zao wanapokua uwanjani, hivyo atatumia siku tano za maandalizi kuwaandaa vyema wachezaji wake ambao wanaonekana kuwa na ari kubwa ya kupambana.
Amesema alianza maandalizi ya mchezo huo muda mrefu, kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na wachezaji aliowaita na kuwaeleza umuhimu wa kupambana ili kupata matokeo.
“Nimewafuatilia wapinzani wetu, hivyo tutawakabili tukiwa tunawafahamu ubora na udhaifu wao” amesema kocha huyo kutoka nchini Burundi.
Wachezaji walioitwa Taifa Stars kwa ajili ya mchezo huo ni Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Adam Adam, Juma Kaseja, Metacha Mnata, Aishi Manula, David Mapigano, Shomary Kapombe, Deus Kaseke, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Brayson David na Bakari Mwamnyeto
Wengine ni Abdallah Kheri, Jonas Mkude, Himid Mao, Erasto Nyoni, Simon Msuva, Ditram Nchimbi, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Ally Msengi, John Bocco, Mzamiru Yassin, Iddy Suleiman, Thomas Ulimwengu, Farid Mussa, Said Mussa, Said Ndemla, Salum Abubakar, Adam Adam na nahodha Mbwana Samatta.