Mashabiki wa soka nchini wameombwa kuendelea kuwa na matumaini na timu yao ya Taifa *Taifa Stars* katika harakati za kusaka tiketi ya kushiriki fainali za afrika (AFCON) 2022.
Wito huo kwa mashabiki wa soka nchini umetolewa na kocha mkuu wa Taifa Stars Etienne Ndayiragije ambaye juzi Jumanne alikiongoza kikosi chake dhidi ya Tunisia na kuambulia matokeo ya sare ya bao moja kwa moja, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema mashabiki wanapaswa kuwa na matumaini makubwa na timu yao, kutokana na nafasi ya kufuzu kupitia Kundi J, kuwa wazi licha ta Tanzania kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo.
“Mashabiki wana nafasi kubwa katika mafanikio ya Taifa Stars, ninawaasa waendelee kuwa kitu kimoja na kuamini timu yao ina nafasi ya kufuzu fainali z Afrika (AFCON) 2022.”
“Bado tuna michezo miwiwli dhidi ya Libya na Guinea ya Ikweta, na baada ya mchezo wetu na Tunisia tumefikisha alama nne, endapo tutashinda michezo iliyobaki ama kupata sare na kushinda mmoja, tutakua na alama ambazo zitakua na sababu ya kutufikisha kwenye lengo letu.”
Kuhusu kupambana kwa wachezaji wa Taifa Stars kwenye mchezo wa juzi Jumanne, kocha Ndayiragije amesema, kila mchezaji aliyepata nafasi ya kucheza dhidi ya Tunisia alipambana kadri ya uwezo wake.
Amesema anawapongeza wachezaji wake kupambana na anaamini kwamba kile ndicho kiwango cha timu yake ilipoishia na kwamba kunahitajika muda mrefu wa kuziandaa timu za taifa kama zinavyoandaliwa klabu za Tanzania katika michezo mikubwa.
“Ukiangalia michezo yote miwili wachezaji wetu wamepambana kuanzia ugenini na nyumbani, sasa tunahitaji kupata maandalizi ya kutosha, nina imani ya kufanya vizuri katika michezo miwili ijayo kupata alama muhimu na kutufanya kusimama katika nafasi nzuri,” amesema Ndayiragije.
Kuhusu mshambuliaji Adam Adam amesema amekiona kitu kwa mchezaji huyo na ana imani ataleta kitu ndani ya kikosi hicho kwa sababu ni mchezo wake wa kwanza a kucheza akiwa ndani ya Stars.
Mchezo ujao kwa Taifa Stars itacheza ugenini dhidi ya Guinea ya Ikweta Machi 22 mwakani, na kisha itacheza dhidi ya Libya jijini Dar es salaam Machi 30 Uwanja wa Benjamin Mkapa.