Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Deogratius J. Ndejembi amezindua jengo la Wagongwa mahututi (ICU), na vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Ndejembi amefanya uzinduzi huo hii leo tarehe Mei 3, 2023 Wilayani humo ambalo ni matokeo ya jitihada za Serikali ya awamu ya sita za kuboresha utoaji wa huduma za afya.
Akiongea katika eneo hilo, Ndejembi amesema “serikali ya awamu ya sita inaendelea kuboreshaji utoaji wa huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na Wilaya Mpwapwa ambapo imejenga Majengo pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya kidigital.”
Amesema Mkoa wa Dodoma umepokea zaidi ya Sh bilioni 1.15 kwa ajili ya ujenzi wa majengo matatu ya huduma za dharura katika wilaya za Kongwa, Bahi na Kondoa, ujenzi unaoenda sambamba na ununuzi wa vifaa tiba vya thamani ya Sh bilioni 1.58.
Aidha, Ndejembi ametoa onyo na tahadhari kwa wizi wa vifaa tiba ambao umekuwa ukijitokeza katika vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo tukio la wiki iliyopita la watumishi wa kituo cha afya katika wilaya Wanging’ombe.
Amewataka Watumishi na Wasimamizi wa huduma za afya kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa Wananchi ili kutimiza lengo la Serikali la kutoa fedha za kujenga majengo na kununua vifaa vya kisasa na kidigitali ili kuboresha utoaji wa huduma.
Kwa Upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (Afya), Dkt. Wilson Mahera amewata watumishi na wasimamizi wa huduma za afya kuhakikisha wanatunza majengo na vifaa tiba ambavyo vimenunuliwa kwa gharama kubwa ili kutoa huduma bora na nzuri kwa Wananchi.
“Viongozi wa wilaya kuweni makini maana kuna baadhi watumishi wanachonga funguo na kuiba vifaa ambapo tumeshakamata watumishi kama wanne wapo chini ya ulinzi waliokuwa wameiba vifaa katika Wilaya Wanging’ombe mkoani Njombe,”amesema Dkt. Mahera.