Spika wa Bunge, Job Ndugai leo ametoa ufafanuzi kuhusu uwepo wa Wabunge 19 wa Viti Maalum kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo bungeni pamoja na kauli alizozitoa Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye kuhusiana na uwepo wa Wabunge hao Bungeni.
Ndugai amesema pamekuwa na maneno mengi ya kumshambulia kwenye mitandao ingawa yeye hapendi kushughulika na mambo ya mitandao.
Ameeleza kuwa wengi wamekuwa wakilisifu Bunge la Tisa lililokuwa chini ya Spika Sitta lakini hawafahamu yeye alikuwa msaidizi wa karibu wa Spika Sitta akihudumu kama Mwenyekiti wa Bunge na ameshiriki kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza kanuni za Bunge zinazotumika sasa.
Ametoa onyo hilo leo Jumatatu Mei 3, 2021 na kuwataka wabunge 19 wa viti maalum ambao wamefukuzwa CHADEMA kuendelea kuchapa kazi kwani wako katika mikono salama.
“Viko vyama vina udikteta, vimejaa mfumo dume, kundi la wanaume linakaa na kuwafukuza wanawake. Wanawake 19 kwa mpigo wanafukuzwa kwa kipeperushi tu. Katiba yao, kuna baraza kuu, hilo baraza kuu limekutana, limefanya uamuzi wa mwisho?” amehoji Ndugai.
“Tabia ya kuonea wanawake lazima iishe katika nchi hii, kwa kupambana na baadhi ya vyama kama hiki cha ajabu ajabu, nani asiyejua hawa mabinti (Halima Mdee na wenzake 18) waliovyopambana. Hata kama barua hiyo inatoka CCM chama changu mnafukuza wabunge wanawake 19 kwa mpigo kwa barua kipeperushi lazima nitawaambia stop kwanza,” amesema Ndugai.
“Unataka tukae tutafute mwafaka wa kitaifa, mwafaka upi Mbowe wakati mwafaka wa chama chako tu unakushinda, unaelewa maana ya mwafaka wa kitaifa? Niwaambie ndugu zangu wa vyama vya siasa, tabia ya kuonea wanawake lazima iishe nchini, kwa kupambana na vyama vilivyojaa mfumo dume kama hiki chama,” amesisitiza Ndugai.