Spika wa Bunge, Job Ndugai amewaagiza Mawaziri kujibu maswali ya Wabunge na kuacha alichokiita majibu ya ‘blabla.’
Spika Ndugai ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Mei 24, 2021 bungeni, alipokuwa akizungumzia kutoridhishwa na namna Mawaziri hao wanavyojibu hoja za Wabunge.
Ndugai amesema wakati wote kiti kimekuwa kikiwavumilia Mawaziri hao kwa kuyaachia majibu hayo yaende kama wanavyojibu.
Awali, kabla ya kuanza kwa kipindi cha maswali bungeni, Spika alionya kwa Mawaziri wenye majibu marefu na wabunge wanaouliza maswali ya nyongeza kwa kuzunguka.
Katika swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Nsimbo, Anna Lupembe ambaye alitaka kujua ni lini Kata ya Ugala itapatiwa umeme baada ya kusubiri kwa muda mrefu, ndipo hapo alipobaini kuwa majibu yaliyotolewa hayakukidhi.
Majibu hayo yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Steven Byabato hayakumridhisha Spika Ndugai, akamuita tena mbele kujibu upya.
Hali hiyo ilimlazimu Waziri wa Nishati, Dk Medad Kalemani kutoa majibu ya nyongeza lakini nayo hayakumridhisha Spika, hivyo akalazimika kumuinua tena Waziri atoe majibu tena.
Majibu aliyoyataka Spika Ndugai ni ya kujua ni lini Kata ya Ugala watapatiwa umeme, Waziri akajibu kuanzia juni mwaka huu, na akaahidi hadi ifikapo mwakani kazi hiyo itakuwa imekamilika.