Taasisi za Serikali zimetakiwa kuona umuhimu wa kuzingatia miondombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kufika kwa urahisi katika maeneo hayo, wanapotafuta huduma katika Taasisi hizo.
Wito huo umetolewa wilayani Kongwa Mkoani Dodoma na Spika wa Bunge Job Ndugai, wakati wa maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu ambayo hufanyika Desemba 3, kila mwaka kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu na kujua mahitaji yao.
Ndugai amesema watu wenye ulemavu mara nyingi wamekuwa wakiachwa nyuma kwenye miondombinu na kuleta usumbufu pindi wanapofika kwenye taasisi hizo kufuata huduma.
Akizungumza kuhusu mikopo ya watu wenye ulemavu, Ndugai amesema licha ya kuwa nao wanatambulika katika kupatiwa mikopo lakini wamekuwa na masharti magumu likiwemo la kuwataka wajiunge katika vikundi vya watu watano.
“Neno vikundi linaleta matatizo makubwa na kupelekea wengine kushindwa kupata mikopo kutokana na masharti yaliyowekwa, haiwezekani watu wenye ulemavu kulazimishwa kuwa katika makundi wakati unakuta katika sehemu moja labda kuna walemavu wawili, sasa kikundi kinataka watu watano,hao wengine wanapatikana wapi, suala hili inabidi tulitazame upya,” amesema Ndugai.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye ulemavu nchini (SHIVYAWATA) Tungi Mwanjala ameiomba Serikali kutoa bure vifaa vya watu wenye ulemavu kutokana na vifaa hivyo kuuzwa bei ghali na hivyo wengi kushindwa kumudu gharama hizo.