Katika kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata elimu ya mpiga kura, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanza maandalizi ya kufanya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 baada ya Serikali kutenga Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya kazi hiyo katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Tume hiyo, Kailima Ramadhani kwa nyakati tofauti wakati akitoa elimu ya mpiga kura katika vituo vya redio vilivyoko mkoani Dodoma.
Amesema kuwa maandalizi ya uboreshaji huo ni pamoja na kutoa elimu ya mpiga kura kupitia vituo vya redio nchi nzima mpango ambao umeanza kutekelezwa kwa baadhi ya mikoa nchini.
“Tume imeanza maandalizi ya kufanya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Serikali imeshatenga Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mwaka 2017/2018”amesema Kailima.
Hata hivyo, ameongeza kuwa kwa kipindi hicho Tume itatoa kadi mpya ya mpiga kura kwa watakaoandikishwa upya, waliopoteza kadi na kadi zilizoharibika, kwa wanaohamisha taarifa zao ikiwemo waliohamia Dodoma, na kufuta wapiga kura waliopoteza sifa za kuwa wapiga kura.