Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imekiri kupokea barua kutoka kwa Mgombea wa Urais kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu akitaka kufanya mkutano wa kampeni huko Somanga, Kilwa.
Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dkt. Wilson Mahera amesema katika barua hiyo Lissu aliomba kufanya mkutano wa kampeni katika eneo la Somanga ambalo kwa mujibu wa ratiba ya NEC kulitakiwa kuwe na mkutano na vyama vingine vya siasa hivyo yalihitajika makubaliano juu ya mabadiliko ya ratiba.
Mahera amesema kuwa kulingana na ratiba ya NEC Lissu alitakiwa kufanya kampeni Lindi , Mtwara na Nachingwea, hivyo Jeshi la Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuzuia mkutano wa kampeni ya mgombea urais Tundu Lissu mjini Somanga.
Lissu katika utetezi wake amedai alikuwa ameandika barua kwa NEC kuomba kibali cha kuruhusiwa kufanya kampeni Somanga kwa sababu hakukuwa na mgombea mwingine aliyepangwa kufanya kampeni.