Kiungo kutoka nchini Nigeria Nelson Esor Okwa amekanusha taarifa za kuwa mbioni kuachana na Simba SC katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo la usajili.
Okwa amekua akitajwa mara kwa mara kuwa kwenye orodha ya wachezaji watakaoachwa ama kuondoka Simba SC kwa mkopo ili kupisha usajili wa wachezaji wengine watakaosajiliwa kipindi hiki.
Kiungo huyo amekanusha taarifa hizo akiwa visiwani Zanzibar ambako Simba SC inashiriki Michuano ya Mapinduzi 2023, na jana Jumanne (Januari 02) usiku ilipoteza 1-0 dhidi ya Mlandege FC.
Okwa amesema hafahamu lolote kuhusu kuondoka klabuni hapo, na badala yake anatambua uwepo wake Simba SC kwa mujibu wa mkataba uliopo kati yake na Uongozi wa Klabu hiyo ya Msimbazi.
“Sifahamu lolote kuhusu kuondoka Simba SC, ninachojua mimi ni mchezaji halali wa klabu hii kwa mujibu wa mkataba uliopo kati yangu na Uongozi, ikitokea ninaondoka kila kitu kitafahamika.”
“Ninaona na kusoma mengi katika Mitandao ya kijamii kuhusu mimi, lakini bado ninasisitiza, Okwa ni mchezaji wa Simba SC na nitaendelea kuwa hapa kwa ajili ya kuipambania Simba SC kwenye Ligi ya ndani na Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.” amesema Okwa.
Mchezaji mwingine anayetajwa sana huenda akaondoka Simba SC ni Kiungo kutoka nchini Nigeria Victor Patrick Akpan, kufuatia kiwango chake kutajwa kuwa cha kawaida, tofauti na alivyofikiriwa aliposajiliwa akitokea Coastal Union.
Tayari Simba SC imeshasajili mchezaji mmoja wa kigeni Saido Nibazonkiza, akiziba nafasi ya Mshambuliaji Dejan Georgijevic aliyevunja mkataba mwezi Oktoba mwaka jana (2022).