Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhana Mgunda amejibu maswali ya baadhi ya Mashabiki wa klabu hiyo kuhusu kutoonekana kwa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Nigeria Nelson Okwa.
Okwa hakuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kilichoikabili Mtibwa Sugar juzi Jumapili (Oktoba 30), katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Kocha Mgunda amesema kutoonekana kwa kiungo huyo, kumetokana na kuwa majeruhi ambayo yalimsababishia kukosa sehemu ya mazoezi ya kuelekea mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar.
Hata hivyo Kocha huyo amesema Okwa anatarajia kuwa sehemu ya kikosi chake siku chache zijazo, kutokana hali yake kuendelea vizuri.
“Wengi wanamuulizia Okwa yupo wapi, kwa sasa yupo nje ya uwanja akiuguza majeraha yake ya misuli, lakini hivi karibuni ataanza kuonekana, kwani ameanza kupata nafuu.”
“Alipata maumivu hayo akiwa mazoezini, hiyo ndio sababu ya kwanza iliyomuondoa katika mchezo wa juzi (Jumapili) dhidi ya Mtibwa Sugar.”
“Kwangu ni jambo la kufurahia, kwani kadri siku zinavyozidi kwenda majeruhi kwenye kikosi changu wanapungua.” amesema Mgunda
Okwa amekua na wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha Simba SC, tangu aliposajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea Rivers United ya nchini kwao Nigeria.