Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Deogratius Ndejembi amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira – NEMC, Mkoa wa Dodoma kufanya ukaguzi na kuwakuchukulia hatua watu wote watakaobainika kutililisha maji machafu ndani mifereji ya barabara na kuchafua mazingira katikati ya Jiji.
Akizungumza katika zoezi la usafi wa mazingira katika kuelekea Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani Juni 5, 2023 Jijini Dodoma, Ndejembi amesema wakati wa zoezi hilo la usafi imebainika kuwa mifereji ya katikati ya Jiji la Dodoma imejaa taka ngumu na maji machafu ambayo ni tishio kwa afya ya binadamu.
Amesema, wapo baadhi ya watu waliopo katikati Jiji hilo wamekuwa na utamaduni wa wakitilisha maji machafu na kutupa taka ngumu katika mifereji ya barabara, hatua inayosababisha mifereji hiyo kwa sasa kujaa taka ambazo zinazoweza kuleta athari mbalimbali kwa wakazi wa maeneo husika ikiwemo magonjwa ya milipuko.
“Naielekeza NEMC kuja kufanya ukaguzi maeneo ya katikati ya Jiji la Dodoma ikiwemo barabara ya Mwanga baa na barabara nyingine za pembezoni na iwapo mtu atabainika kutililisha maji machafu au taka ngumu kutoka katika nyumba yake au biashara yake hana budi kuwachukulia hatua za kisheria” amesema Ndejembi.