Aliyekau nahodha na beki wa pembeni na Manchester United Gary Neville amesema kikosi cha klabu hiyo kinahitaji kuongezewa baadhi ya wachezaji kwa haraka, ili kuimarisha makali yake kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya England.
Manchester United watafungua msimu wa Ligi Kuu ya England Septemba19, kwa kupapatuana na Crystal Palace, lakini Neville haamini kama wana kikosi kitakachoanza vyema mshike mshike huo.
Neville amesisitiza kupatikana kwa wachezaji haraka katika dirisha hili la uhamisho na kugusia vita ya David de Gea na Dean Henderson kwenye kikosi cha meneja Ole Gunnar.
Gwiji huyo amesema mpaka sasa, Manchester United haina uwezo wa kuleta ushindani kwenye Ligi Kuu ya Uingereza kwa msimu ujao, kutokana na uwepo wa wachezaji kwenye kikosi chao.
Wataalamu wa soka, wanakitazama kikosi cha Manchester United kama kikosi ambacho kinahitaji nyongeza ya wachezaji wanne ama watano hivi ili kiwe na mtazamo wa ushindani.
Manchester United walijaribu kumsajili Jadon Sancho Borrusia Dortmund, lakini mambo yaliwaendea kombo kutokana na ada ya mchezjai huyo wa England kuwa kubwa, tofauti na walivyofikiria.
Wakati dirisha la usajili likielekea kufungwa mapema mwezi Oktoba, Manchester United wanahitaji kuutumia muda huo vizuri, ili kujiweka katika nafasi ya kuboresha kikosi na kushindana kwenye Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Ulaya.