Magwiji Gary Neville na Jamie Carragher wamekubaliana kwenye majina ya wachezaji sita wakati walipotaja vikosi vyao bora kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Magwiji hao wawili ni kawaida yao kutokubaliana, lakini hakuwa na mjadala katika ishu ya kuwataja mastaa Erling Haaland na Kevin De Bruyne kwenye vikosi vyao vya msimu.
Mastaa hao, sambamba na wachezaji wenzao Ruben Dias na Rodri wameisaidia Manchester City kutetea taji lao la Ligi Kuu England na kulibeba kwa msimu wa tatu mfululizo na wakali hao wote wanne wametajwa kwenye vikosi vya Neville na Carragher.
Wachambuzi hao wamekubaliana pia, nahodha wa Arsenal, Martin Odegaard naye anastahili kuwamo kwenye vikosi vyao vya msimu baada ya kufunga mabao 15 na kuasisti mara nane kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Lakini, Neville na Carragher walitofautiana kwa wachezaji wengine wa Arsenal, na Carragher kwenye kikosi chake alimtaja Oleksandr Zinchenko kwenye beki ya kushoto.
Neville aliamua kumchagua mkali wa Brighton, Pervis Estupinan kwenye beki na kushoto na huko Arsenal, alikwenda kuwaongeza wakali wengine wawili kwenye kikosi chake, Bukayo Saka ana Gabriel Martinelli.
Carragher fowadi yake amewachagua Harry Kane na Mohamed Salah huku golini akimtaja Liverpool, wakati Neville kipa wake ni Nick Pope na beki wake wa kati ni William Saliba.
Wachambuzi hao walikubaliana pia kwa beki wa kulia Kieran Trippier kutokana na kiwango chake cha msimu huu, Carragher akimtaja Sven Botman kuwa ni beki wake wa kati.
Mashabiki wengi walimpongeza Neville kutaja kikosi kizuri, lakini walishtuka kwa kutomtaja staa yeyote wa Manchester United, ambapo mmoja aliandika: “Man United ipo Top Four. Lakini, haina hata mchezaji mmoja, huu ni mzaha.”