Rapa Ney wa Mitego Jana alijikuta katika mvutano na mtu anayesadikika kuwa ni Askari Kanzu baada ya kumpiga picha za Video yeye na gari lake bila idhini yake katika kituo cha polisi cha Osterbay Jijini Dar es salaam.
Tukio hilo liliibuka wakati Ney akiwa ni miongoni mwa watu waliofika katika kituo hicho kusubiri hatma ya msanii Roma Mkatoliki na wenzake waliokuwa wakihojiwa kufuatia tukio la kutekwa kwao na kupatikana.
Dar24 ilishuhudia tukio hilo la mvutano, ambapo Ney alimng’ang’ania mtu huyo aliyekuwa anamrekodi yeye na gari lake, ambapo mvutano huo ulishuhudiwa pia na waandishi wa habari wengine waliokuwa wametanda katika eneo hilo na ulimalizika baada ya mtu huyo anaesadikika kuwa ni askari kukubali kufuta picha zote alizochukua.
Katika hatua nyingine, Ney alieleza kuwa hakuweza kula kwa siku mbili tangu alipopata taarifa za kutekwa kwa Roma na wenzake hadi alipopata taarifa za uhakika jana kuwa wamepatikana.
Baada ya tukio hilo Mama mzazi wa msanii Moni ambaye ni miongoni mwa waliotekwa na kupatikana, Fatma Saleh Awadhi alisema kuwa amesikitishwa sana na kitendo alichofanyiwa mwanae na kuongeza kuwa hataki tena mwanae afanye muziki.
Hata hivyo, Roma alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa wako salama kiafya na kuahidi kuelezea tukio hilo kiundani zaidi siku ya jumatatu