Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Brazil, Neymar da Silva Santos Júnior ameripoti leo polisi jijini Rio de Janeiro kwa ajili ya kutoa maelezo na kuhojiwa kuhusu tuhuma za ubakaji.
Wiki iliyopita, mrembo Najila Trindade alimtuhumu mshambuliaji huyo wa Paris Saint-Germain (PSG) kuwa alimbaka Mei 15 katika hoteli moja jijini Paris nchini Ufaransa.
Trindade alifunguka zaidi kupitia kipindi cha runinga nchini Brazil akidai kuwa mchezaji huyo alimuingilia bila ridhaa yake na akaomba hatua stahiki zichukuliwe.
Kutokana na tuhuma hizo, MasterCard walitangaza kuvunja mkataba wa matangazo na mchezaji huyo aghali zaidi duniani ikiwa ni pamoja na kuondoa picha yake kwenye kampeni zao.
Kadhalika, kampuni ya Nike Inc ambayo ni wadhamini wa Neymar imeeleza kupitia tamko lake kwa vyombo vya habari kuwa wanayazingatia sana na wanafuatilia kwa karibu tuhuma za ubakaji.
Neymar amekana tuhuma hizo dhidi yake.
Mwanasheria wake, Maira Fernandes ameiambia Reuters kuwa Neymar emewaeleza polisi kwa undani kuhusu tuhuma hizo.
“Tunaamini kuwa mteja wetu hana hatia, utaratibu unaendelea kukamilika lakini tunatoa ufafanuzi ambao ulipaswa kutolewa,” alisema Fernandes.
Akizungumza nje ya kituo cha polisi baada ya kutoa maelezo, Neymar alisikika akisema, “ninashukuru kwa kuniunga mkono na jumbe ambazo dunia nzima imetuma, marafiki, mashabiki, kwamba dunia iko na mimi. Ninapenda kusema kuwa ninashukuru kwa kunitakia kheri.”