Wakati tetesi za usajili zikieleza huenda mshambuliaji kutoka nchini Brazil Neymar da Silva Santos Júnior akarejea FC Barcelona, mgombea urais ndani ya klabu hiyo ya Hispania Victor Font, amesema endapo atapata nafasi ya kuongoza, hatokua na nafasi ya kumfikiria mchezaji huyo.
Neymar ambaye aliachana na FC Barcelona mwaka 2017 na kutimkia kwa mabingwa wa Ufaransa Paris Saint-Germain (PSG), anahusishwa na taarifa hizo mara kwa mara, lakini Font ameamua kujilipua na kuliingiza suala hilo kwenye kampeni zake.
Amesema mshambuliaji huyo alieondoka klabuni hapo kwa ada ya usajili iliyovunja rekodi mwaka 2017 ya Euro Milioni 222, hatokua sehemu ya mipango yake, aliyoiandaa kwa ajili ya kukiboresha kikosi cha Barca.
“Kikatiba Neymar hayupo kwenye mipango yangu,” Font alisema ambaye kipindi cha nyuma alisema atamrudisha Pep Guardiola katika klabu hiyo kuungana na Messi.
“Kwa sababu za kiuchumi na sababu nyingine za kisheria alikuwa dhidi ya klabu na ukweli ni kwamba aliiacha klabu katika hali ngumu kabla msimu haujaanza mwaka 2017.
“Atafaa katika upande wa michezo lakini siyo kwenye uchumi au upande wa mambo ya taasisi,” Font aliongeza kwenye mahojiano na Sport
“Lakini masuala ya usajili yataendelea kuwa katika mikono ya bodi ya klabu, ambao bado haujafanyika mpaka sasa.
Neymar amefunga mabao 49 katika michezo 56 katika ligi ya Ufaransa tangu alipoanza kuitumikia Paris Saint-Germain na kutoa pasi za mwisho 29, huku akiwa mchezaji pekee alieshirikiana na mshambuliaji mwenzake Kylian Mbappe ambaye amehusika kwenye mabao 95 kwenye ligi hiyo.
Alipokua FC Barcelona kuanzia mwaka 2013-2017, mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kuwa nahodha wa timu ya taifa ya Brazil, alihusika moja kwa moja kwenye mabao 164 katika michezo 186 na kuisadia klabu hiyo kushinda mataji manane.
Nafasi ya Urais FC Barcelona kwa sasa ipo wazi, tangu Josep Maria Bartomeu alipotangaza kujiuzulu mwishoni mwa mwezi Oktoba, kufuatia wanachama kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Font yupo katika nafasi kubwa ya kushinda kinyang’anyiro hicho na uchaguzi uanatarajiwa kufanyika Januari 24 mwaka ujao.