Mshambuliaji kutoka nchini Brazil Neymar da Silva Santos Júnior amesema alilia kwa siku tano mfululizo baada ya Timu yake ya Taifa kutolewa katika mashindano ya Kombe la Dunia 2022 na kuongeza alifikiria kustaafu kucheza kimataifa baada ya kushindwa kwenye hatua ya Robo Fainali dhidi ya Croatia.

Mshambuliaji huo wa Klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa, mwenye umri wamiaka 31, hajaichezea nchi yake tangu kupoteza kwa Penalti Desemba 9, mwaka jana.

Neymar aliiweka Brazil mbele kwa kile kilichoonekana kama bao la ushindi katika muda wa nyongeza kabla ya Croatia kusawazisha zikiwa zimesalia dakika tatu na kushinda mikwaju hiyo na kutinga nusu fainali.

“Siwezi kukwambia kilichopita kichwani mwangu.” alisema Neymar akiiambia YouTuber Casimiro

“Kulikuwa kushindwa kwa uchungu zaidi katika maisha yangu, kwa hakika nililia kwa siku tano mfululizo. lliniumiza sana, ndoto yangu ilikuwa imebadilika. Tukiwa 0-0 nilifunga bao, walisawazisha na tukapoteza kwa Penati. Ni maumivu ambayo wachezaji na wafanyakazi pekee wanaweza kuelewa.

“Ulikuwa wakati mbaya zaidi maishani mwangu. Ilionekana kama mazishi, mtu analia upande, mtu mwingine akilia upande mwingine. Ilikuwa hali ya kutisha, hisia ile sitaki kuiona tena.”

Neymar ameichezea Brazil katika fainali tatu za Kombe la Dunia akianza mwaka 2014, 2018 na 2022.

Mwaka 2014 waliadhibiwa 7-1 na Mabingwa Ujerumani katika Nusu Fainali kwenye ardhi ya nyumbani kwao baada ya Mshambuliaji huyo kuumia mgongo katika Hatua ya Makundi.

Miaka minne baadae nchini Urusi, Brazil ilichapwa 2-1 na Ubelgiji katika Robo Fainali kabla ya kuondolewa katika hatua kama hiyo na Croatia nchini Qatar mwaka 2022.

Katika mahojiano na CazeTV, Neymar alisema alikuwa akifikiria kustaafu kimataifa baada ya kukatishwa tamaa, lakini sasa yuko tayari kucheza tena 2026.

Baada ya Kombe la Dunia (2022), kwa kweli sikutaka kurejea katika timu ya taifa ya Brazil,” alisema.

“Lakini nimebadilisha mawazo yangu. Kwa sababu nina njaa sana. Nilibadilisha mawazo yangu.

“Baada ya Kombe la Dunia, sikutaka kupitia uchungu wa kupoteza tena. Kuona familia yangu ikiteseka sana, hilo linanielemea sana. Lakini itabidi wavumilie tena. Itakuwa vizuri. Lazima iwe hivyo Kampeni ya Brazil ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 itaanza Septemba mwaka huu.

Shirikisho la soka la Brazil, CBF, limemteua Fernando Diniz wa Fluminense kama kocha wao mpya wa muda kwa mkataba wa mwaka mmoja, huku wakimfuatilia Carlo Ancelotti wa Real Madrid kama uteuzi wa muda mrefu.

Neymar amerejea katika mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya na PSG, ambayo sasa inafundishwa na kocha wake wa zamani kule Barcelona, Luis Enrique.

Jana Ijumaa (Julai 21) walicheza na Le Havre katika mechi ya kirafiki kabla ya kuondoka kwa ziara nchini Japan ambako watacheza na Al Nassr, Cerezo Osaka na Inter Milan.

Mkaguzi chakula cha Rais afichua jambo
Utoaji wa Habari uzingatie vyanzo vya kuaminika - Nape