Kiungo Mshambuliaji wa zamani wa Klabu za Simba SC na Young Africans Mrisho Khalfan Ngassa amezishauri klabu hizo kuelekea Michezo ya Mkondo wa Pili ya Robo Fainali ya Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Simba SC leo Ijumaa (Aprili 28) itacheza mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Wydad AC itakayokuwa nyumbani mjini Casablanca nchini Morocco, huku Young Africans ikitarajia kucheza mchezo wa hatua hiyo katika Michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mabingwa wa Nigeria Rivers United, Jumapili (Aprili 30) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Ngassa amesema timu zote zina nafasi ya kufuzu hatua ya Nusu Fainali kwenye michuano hiyo ya CAF lakini upande wa Simba SC watakutana na ugumu kutokana na namna Waarabu wanavyocheza wanapokuwa katika viwanja vya nyumbani.
“Mpira ni dakika 90 lakini ndani ya hizo dakika unatakiwa kuangalia na kuongeza umakini zaidi juu ya mpinzani wako, Young Africans wamecheza na timu ambayo inaonekana kama ina tatizo kidogo lakini hiyo isiwe kigezo cha kuuchukulia mchezo huo kama wa kawaida kwao, wanaweza kuja kivingine, wapambane kama ni mechi ya kwanza.”
“Simba SC wanaenda kukutana na timu ambayo inajua kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani, ila naamini kama watakuwa makini na mbinu zao watashinda,” amesema Ngassa
Mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Simba SC ilishinda 1-0, huku Young Africans ikipata ushindi wa 2-0 ugenini Nigeria.