Usiku wa kuamkia leo, Aprili 26, 2020 vyombo vya habari hasa vya Magharibi vimeripoti kuwa huenda Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un amefariki dunia.
Taarifa hizo zimekuja ikiwa ni siku chache tangu kuwepo na taarifa kuwa kiongozi huyo yuko mahututi kutokana na kufanyiwa upasuaji wa moyo ambao haukuwa na mafanikio.
Ilielezwa kuwa wiki hii, timu ya madaktari kutoka nchini China ilienda Korea Kaskazini kwa ajili ya kusaidia kumpa huduma za matibabu kiongozi huyo, lakini haikuelezwa wazi kuhusu hali yake.
Kwa mujibu wa ripoti ya vyombo vya upelelezi vya Marekani zilizotolewa Jana, Aprili 25, 2020 zikiwa na picha za setelaiti, treni ya kiongozi huyo ilionekana katika kituo chake kilichopo Wonsan kati ya Aprili 21 na Aprili 23. Kituo hicho ni maalum kwa familia ya Kim.
Hata hivyo, vyombo hivyo vya upelelezi vya Marekani vinavyochunguza ndani Korea Kaskazini, vimekaririwa vikieleza kuwa havioni dalili zozote za mabadiliko ya shughuli za kijeshi nchini humo wakati taarifa hizi zikiendelea kusambaa.
Tetesi za afya ya Kim kuzorota ziliibuka baada ya kukosa kwa mara ya kwanza kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa babu yake.
Lakini pia baada ya kukosa sherehe nyingine ya kitaifa kwa namna ambayo sio utamaduni wake, zimeibuka taarifa kuwa huenda kiongozi huyo amefariki dunia. Kim hajaonekana hadharani kwa kipindi cha wiki mbili sasa, na Serikali ya nchi hiyo haijatoa tamko lolote kuhusu tetesi zinazoendelea.
Hakuna chombo kilichothibitisha kuwa amefariki dunia. Lakini leo vyombo vingi vya Magharibi vimemnukuu Makamu Mkurugezi wa Kampuni inayomiliki vyombo vya habari nchini China (HKSTV Hong Kong Satellite Television), Shijian Xingzou anayesadikika kuwa ni mpwa wa Waziri wa Mambo ya Nje wa China, akieleza kuwa amepata taarifa kutoka kwa chanzo cha ndani na cha kuaminika kuwa Kim Jong-un amefariki dunia.
Taarifa nyingine zilizoripotiwa na gazeti la Japan la Shukan Gendai zimemkariri daktari waliyedai alikuwa mmoja kati ya madaktari waliotumwa kutoka Pyongyang, China kumtibu Kim Jong-un, akisema kiongozi huyo kweli yuko mahututi.
Hata hivyo, Alhamisi wiki hiii, Rais wa Marekani, Donald Trump alikaririwa kuwa anaamini taarifa kuhusu hali tete ya afya ya Kim Jong-un na taarifa nyingine zinazoendelea kusambazwa na vyombo vya habari ikiwemo CNN sio sahihi.
“Sijui, mimi nina uhusiano mzuri na yeye, sijui… kama ni kweli yasemwayo hiyo ni hali ngumu sana, lakini ninamtakia heri…. Tuna uhusiano mzuri. Nimeshasema na ninasema tena sasa hivi kama mtu mwingine angekuwa kwenye hii nafasi [ya Urais wa Marekani sasa hivi] tungekuwa vitani na Korea Kaskazini, na tulikuwa karibu kuingia vitani na Korea Kaskazini. Kwahiyo, ninamwambia Kim Jong-un ‘namtakia heri,” Trump amewaambia waandishi wa habari, Aprili 23.
“Wamekuja na ripoti nzito ya matibabu, hakuna ambaye ameithibitisha…. CNN wanapokuja na ripoti yao huwa siweki imani yangu hapo.” Aliongeza.
Alisema watu walitegemea akiingia madarakani tu Marekani itapigana vita nyingi ikiwemo dhidi ya Korea Kaskazini, lakini hakuna kitu kama hicho sasa na kwamba hataki kuwa polisi wa dunia.
Furaha kwa baadhi ya viongozi wa Marekani:
Ingawa taarifa za kifo cha kiongozi huyo ni taarifa za huzuni, baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa Marekani wameonesha dhahiri kufurahi endapo itakuwa kweli.
Seneta Mwandamizi wa Jimbo la Carolina Kusini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Haki ya Seneti, Lindsey Graham ameeleza kufurahishwa endapo taarifa hizo zitakuwa sahihi.
Amesema atapata mshtuko endapo habari za kifo cha Kim Jong-un hazitakuwa sahihi kwa sababu haiwezekani Serikali ya Korea Kaskazini ingawa ni nchi iliyojificha sana ikashindwa kuzungumzia taarifa nzito kama hizo.
Aliongeza kuwa anaamini taarifa hizo ni za kweli na kwamba sasa Marekani na Korea Kaskazini watakuwa na wakati mzuri zaidi wa ahueni ya maisha na kufanya biashara na mrithi wake.
“Tuna imani sana kuwa amekufa au kweli yuko mahututi. Na kwa maana hiyo natumaini mateso ya muda mrefu kwa watu wa Korea Kaskazini yatakuwa yamepata ahueni,” Washington Examiner linamkariri Seneta Graham.
“Rais Trump amekuwa akionesha nia ya kufanya biashara na Korea Kaskazini katika mtindo ambao wote tunafaidika (win-win). Sasa kama huyu jamaa amefariki dunia, ninatumaini anayekuja kumrithi atafanya kazi na Rais Trump kuifanya Korea Kaskazini kuwa sehemu bora zaidi kwa kila mmoja,” aliongeza.
Kim Jong-un anadaiwa kuwa na matatizo ya moyo, huku ikikumbukwa kuwa baba yake, Kim Jong-il alifariki mwaka 2011 kwa ugonjwa wa moyo.