Mara baada ya Young Africans kufikia hatua nzuri ya kumsajili kiungo Fabrice Ngoma kutoka Al Hilal Omdurman ya nchini Sudan, imebainika kwamba klabu hiyo imeanza mpango wa kufanya usajili wa mshambuliaji mwingine kutoka DR Congo, Makabi Lilepo akitajwa kwamba ndiye atakuwa mrithi sahihi wa Fiston Mayele.
Young Africans tayari wameweka wazi mipango yao ya kuhakikisha msimu ujao wanafanya vema katika michuano ya kimataifa ambapo watashiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Msimu huu wa 2022/23, Young Africans ilianzia Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini ilipoteleza, ikaangukia Kombe la Shirikisho barani humo na kufika hadi fainali, lakini kwa bahati mbaya ilishindwa kutwaa Ubingwa mbele ya USMA kwa kanuni ya bao la ugenini.
Chanzo cha kuaminika kutoka DR Congo, kimeeleza mpango wa Young Africans wa kukamilisha usajili wa wachezaji hao wote wawili kutoka Al Hilal Omdurman, licha ya Simba SC nayo kumuhitaji Makabi Lilepo.
“Young Africans baada ya kufikia pazuri kwenye usajili wa Fabrice Ngoma, sasa wamehamishia nguvu zao kuhakikisha wanamsajili Makabi Lilepo ambaye wanaamini wakimpata utakuwa usajili mzuri kwao kutokana na uchezaji wake kuendana na Klabu hiyo.
“Young Africans wanafahamu kuwa Simba SC wapo kwenye mazungumzo na Lilepo, lakini wanachokifanya ni kuamini katika mpango wao, hivyo kwa sasa ninavyokwambia klabu hiyo mpango wake ni kuwapata wachezaji hao wote wawili raia wa DR Congo.
“Wote ni wachezaji ambao wanapatikana kwa sasa kutokana na hali ilivyo nchini Sudan, ambako Ligi imesimama, hivyo uongozi wa Al Hilal upo tayari kusikiliza ofa za wachezaji, ni suala la viongozi wa timu husika kupeleka ofa,” kimesema chanzo hicho.