Hatimaye Uongozi wa Young Africans umethibitisha kupokea ofa na kumuachia Kiungo Kutoka Visiwani Zanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutimkia Azam FC, baada ya mzozo wa muda mrefu.

Uongozi wa klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ulikua na msuguwano na Kiungo huyo kwa muda mrefu, kufuatia Fei toto kushinikiza kuvunjwa kwa mkataba wake, lakini aligonga mwamba zaidi ya mara moja mbele ya Kamati ya Sheria na hadi za wachezaji ya TFF.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Young Africans, ofa hiyo imetumwa baada ya kukamilishwa kwa mazungumzo kati yao na Feisal kufuatia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa juzi Jumanne (Juni 05) wakati wa hafla ya kuipongeza klabu hiyo baada ya kufika Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Taarifa ya Young Africans imeeleza: Uongozi wa Young Africans Sports Club unapenda kuutarifu umma kuwa umepokea ofa kutoka Klabu ya Azam FC ya kumuhitaji mchezaji Feisal Salum.

Baada ya mazungumzo ya pande zote mbili na kwa kuzingatia matakwa ya kimkataba kati ya Klabu na Mchezaji, Uongozi wa Young Africans Sports Club umefikia uamuzi wa Kumuuza mchezaji huyo kwa Klabu ya Azam FC.

Mchezaji Feisal Salum ameuzwa kwenda Azam FC kwa dau ambalo halitawekwa wazi kutokana na makubaliano ya pande zote mbili.

Feisal ataungana na timu yake mpya baada ya makubaliano binafsi na dirisha la usajili kufunguliwa rasmi.

Uongozi wa Young Africans Sports Club unamtakia kila la kheri Feisal Salum katika majukumu yake mapya.

Galtier afunguliwa mlango wa kutokea PSG
Serikali haijasaini mkataba wa miaka 100 - Mkurugenzi TPA