Jeshi la Nigeria limeanza kujenga barabara inayopita ndani ya msitu wa Sambisa ambao ni ngome kuu ya kundi la kigaidi la Boko Haram.
Msitu huo wenye kilometa za mraba 686 kaskazini mwa Jimbo la Borno unaaminika kuwa ndiyo sehemu alipojificha kiongozi mkuu wa Boko Haram, Abubakar Shekau. Kwa mujibu wa taarifa za jeshi, barabara hiyo itaunganisha miji kadhaa.
Ujenzi huo tayari umeanza katika eneo la Gwoza-Yamteke-Bitta-Tokumbere ukielekea katika msitu huo.
Msemajiji wa jeshi la Nigeria, Sani Kakusheka Usman amesema kuwa jeshi hilo limepanga kugeuza msitu huo kuwa sehemu maalum ya mafunzo ya wanajeshi wake.
Amesema kuwa ujenzi huo utasababisha barabara kadhaa kufungwa hadi Februari 4 mwaka huu wakati ambapo shughuli za matayarisho zikiendelea.
Ingawa jeshi hilo limekuwa likitangaza mara kadhaa kuwa limewafuta Boko Haram, kundi hilo la kigaidi limekuwa likishtukiza na kufanya mashambulizi yenye madhara makubwa kwa watu wasio na hatia.