Beki wa Young Africans Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amesema wanatamani kuchukua mataji mawili tena kwa kuichapa Simba SC na anaamini jambo hilo litatimia watakapokutana Julai 25 kwenye Fainali Kombe la Shirikisho (ASFC).
Mara ya kwanza mwaka huu Young Africans iliichapa Simba SC kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa changamoto ya Penati 5-4, baada ya kwenda sare ya 0-0 ndani ya dakika 90, na kufanikiwa kutwaa taji la Michuano hiyo ambayo ni sehemu ya ‘SHAMRA SHAMRA’ za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Ninja ambaye hakuwa sehemu ya kikosi kilichoikabili Simba SC Julai 03, Uwanja wa Benjamin Mkapa amesema, wamedhamiria kushinda mchezo huo na wanaamini inawezekana.
Amesema mchezo utakua mgumu kutokana na Simba SC kuhitaji kulipa kisasi cha kupoteza mchezo uliopita, lakini bado akasisitiza ushindi katika pambano hilo ni lazima.
“Sina maana kwamba mchezo utakuwa rahisi hapana, ila ushindani utakuwa wa hali ya juu, lakini lengo letu ni kuhakikisha taji hilo linakwenda Jangwani,” amesema Ninja.
Katika hatua nyingine Beki huyo kutoka visiwani Zanzibar, amesema japokuwa ameikosa baadhi ya michezo kutokana na kusumbuliwa na majeraha, anaamini Young Africans ina wachezaji wapambanaji ambao wakiamua kwa nia moja wanaweza wakafanya maajabu katika mchezo huo.
“Young Africans ni jeshi kubwa ambalo linaweza likabadili upepo kama tulivyobadili wakati ambapo waliona Simba ina nafasi kubwa ya kushinda mchezo wa mzunguko wa pili, lakini tukawafunga wakawa wapole, ndivyo itavyoweza kuwa hata Kigoma,” amesema Ninja.
Young Africans ilitinga Fainali ya Kombe la Shirikisho kwa kuichapa Biashara United Mara bao 1-0, Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi mkoani Tabora, huku Simba SC ambao ni Mabingwa watetezi wakifanya hivyo kwa kuibamiza Azam FC bao 1-0, Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma mwishoni mwa mwezi Juni.