Serikali imeshauriwa kuweka utaratibu mzuri wa kibiashara kwa wauzaji wa nishati ya gesi ili waweze kuyafikia maeneo mengi hasa ya vijijini.
Hayo yamebainishwa hii leo Novemba1, 2022 na Prof. Anna Tibaijuka wakati alipokuwa akichangia mada wakati wa ufunguzi mjadala wa kitaifa wa Nishati safi ya kupikia unaofanyika kwa siku mbili (Novemba 1-2, 2022) jijini Dar es Salaam.
Amesema sehemu kubwa ya wananchi wa Vijijini wamekuwa wakikumbana na adha ya utafutaji wa kuni kwa ajili ya kupikia kitu ambacho kimekuwa kikiwapotezea muda mwingi wa kufanya shughuli za kuinua vipato vyao na hivyo kushindwa kumudu gharama za maisha.
“Mimi mwenyewe ni muhanga wa watu walikuwa wakikumbana na adha ya utafutaji kuni hivyo naelewa fika suala hili kama kweli mjadala huu unalenga kuleta unafuu ni wazi kwamba tunahitajika kuchukua hatua rafiki kwa kuwashirikisha Wafanyabiashara wa gesi,” amefafanua Tibaijuka.
Hata hivyo ameishauri Serikali pia kuangalia gharama za upandaji wa vitu mbalimbali na kuziweka katuka hali rafiki kwa kila nyanja ili kuepuka kuleta nafuu ya jambo moja huku mengine yakiendelea kuwakandamiza wananchi.
Amesema, ipo haja pia ya kuwazua jinsi ya kukishughulikia jambo hilo la nishati safi ya kupikia upande wa gharama kwani matumizi ya mkaa ni rahisi kutokana na wafanya biashara kuweka mazingira rafiki kwa kuuza mafungu kulingana na hali ya Wananchi.