Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimezungumzia taarifa kuhusu anayetajwa kuwa mhadhiri wa chuo hicho, Samson Mahimbo aliyepandishwa jana kizimbani akikabiliwa na mashtaka ya kumuomba rushwa ya ngono mwanafunzi ili amsaidie kufaulu masomo.
Afisa Mahusiano kwa Umma wa NIT, Ngusekelo David amesema kuwa Mahimbo sio mhadhiri wa chuo hicho kwa sasa na kwamba mkataba wake uliisha miezi mitatu baada ya kukamatwa kwa tuhuma hizo.
“Mkataba wake uliisha kwetu tangu 2017, alikuwa Mhadhiri wetu wa muda (part time), kipindi hicho alichokuwa amepata hizo kashfa ilikuwa imebaki miezi mitatu tu mkataba wake kuisha, kwahiyo ulipoisha hatukumpa mkataba mwingine,” Bi. David aliimbia Clouds Fm.
“Lakini sio kwamba tunamkana… ni kweli kwamba yule sio mhadhiri wetu tena, na ni yeye pekee ambaye amekuwa na kashfa hizo na hata sisi tumeshangazwa na alichofanya,” aliongeza.
Jana, Agosti 14, 2019 Mahimbo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, ambapo mwanasheria kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Vera Ndeoya aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa alifanya kosa hilo Januari 12, 2019 katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Com David iliyoko Mwenge jijini humo, akiwa mwajiriwa wa NIT.
Mahimbo alikana mashtaka hayo na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.
Wakili wa Takukuru aliieleza mahakama kuwa ushahidi wa kesi hiyo umekamilika. Hakimu aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 17, 2019 itakapoanza kusikilizwa.